Semantics and Pragmatics in Kiswahili

Leon Ike Oduor                                 


UTANGULIZI.


v  Maana ya semantiki kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali.


v  Maana ya pragmatiki kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. 


KIINI.


v  Uhakiki kwa kutumia mifano mbalimbali katika lugha ya Kiswahili juu ya ukweli wa dai kuwa,pragmatiki huanzia pale ambapo semantiki huishia.


 


            Katika kujibu swali hili tutaanza na kufafanua dhana za msingi zilizo jitokeza katika swali letu kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali dhana hizo ni pamoja na; semantiki na pragmantiki. Baada ya kuzifasili maana hizo tutajikita kwenye kiini cha swali kuwa pragmantiki huanzia pale ambapo semantiki huishia  kisha tutahitimisha mjadala huu na mwisho tutaorodhesha marejeo.


Kwa kuanza na kufafanua maana ya semantiki ; wataalamu mbalimbali wanaeleza maana ya semantiki kwa namna tofautitofauti kama ifuatavyo;


Alfred (1933), anaeleza kuwa semantiki ni Nyanja inayojishughulisha na uchambuzi wa maana.


Naye Yule (1996),anamuunga mkono Alfred kwa kufafanua maana ya semantiki kuwa inajihusisha na uchambuzi wa maana katika neno na katika sentensi.


Pia Stuwart na Nathan (2001), na Habwe na  Karanja (2004),wanafanana katika kuwafasili maana ya semantiki isipokuwa wanatofautiana katika istilahi kwani Stuwart na Nathan wanatumia dhana ya tawi la isimu wakati Habwe na Karanja wanatumia istilahi ya utanzu wa isimu. Lakini wote wanafafanua kuwa semantiki inajihusisha na uchambuzi wa maana katika lugha.


Hivyo basi kwa ujumla tunaweza kusema kwamba semantiki ni tawi la isimu linalojishughulisha na uchunguzi wa maana katika lugha za binadadamu.


Pamoja na wataalamu hawa kujishughulisha na maana ya semantiki, hawakuishia hapo tu  kwani walijishughulisha pia na maana ya pragmantiki kama inavyoelezwa hapa chini.


Bakari (1988) anaelaza kuwa pragmantiki ni maana ambapo mwandishi au msemaji amekusudia kuiwasilisha. Maana hii inatokana na muktadha wa mwadishi au msemaji.


            Maana hii kwa kiasi Fulani imeonekana kuwa na udhaifu Fulani kwani anajikita zaidi katika muktadha wa msemaji au mwandishi kumbe basi pragmatiki ni sharti izingatie pia muktadha wa hadhira yaani msomaji na msikilizaji na sio muktadha wa msemaji au mwandishi tu.


Stuwart na Nathan (2001) wao wameenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa pragmantiki inajihusisha na namna watu wanavyotumia lugha katika muktadha na kwa nini wanatumia lugha kwa namna hiyo.


Hivyo tunaweza kusema kuwa pragmantiki ni stadi inayochunguza maana kulingana na muktadha Fulani.


            Baada ya kufafanua maana ya semantiki na pragmatiki , ufuatao ni uhakiki wa dai kuwa pragmantiki huanzia pale ambapo semantiki huishia. Ni dhahiri kuwa pragimantiki huanzia pale ambapo semantiki huishia kutokana na nyanja za maana kama vile maana ya msingi na maana ya ziada. Kwa sababu pragmantiki imekuwa kama suluhisho la mapungufu ya semantiki yaani pale ambapo semantiki imeshindwa kuelezea pragmantiki huendeleza; hii ni kutokana na ukweli kwamba semantiki huelezea maana ya msingi tu ya neno au sentensi wakati pragmantiki huelezea maana ya ziada. Ufuatao ni uthibitisho wa dai kuwa pragmantiki huishia pale ambapo semantiki huishia,kwa kuangalia mambo yafuatayo:


            Maana na matumizi ya maneno; semantiki hueleza maana ya msingi lakini neno hilohilo linaloelezwa kisemantiki linapokuwa katika matumizi ndipo tunapata maana ya ziada ambayo ndio pragmantiki.


Mfano;


Neno simba ni mnyama mkali mwenye rangi ya majani makavu anayeishi porini.


Neno hilohilo simba linapokuwa katika matumizi linatupatia maana tofauti na ile ya msingi ambayo ndiyo maana ya kipragmantiki.


Mfano; Hakika kijana Yule ni simba kwelikweli; kinachomaanishwa hapa sio kijana Yule ni mnyama kama semantiki inavyoeleza bali kinachomaanishwa ni kuwa kijana Yule ana tabia kama za simba kwa maana kuwa ni mkali , hodari na ana nguvu sana. Hivyo tunaona kuwa pragmantiki inaenda mbali zaidi kutoka pale ambapo semantiki inaishia.


            Matumizi ya methali mbalimbali, Methali ni semi fupifupi zenye kueleza kwa muhtasari fikra au mafunzo mazito yanayotokana na uzoefu wa kijamii. Katika kuangalia methali tunaangalia maana ya kisemantiki na ya kipragmatiki mfano methali kama 


“mgaagaa na upwa hali wali mkavu”.  katika methali hii maana ya msingi (maana ya kisemantiki) ni kuwa mtu anayezunguka katika ufukwe wa bahari hawezi kula wali mkavu. Hapa tunaona pragmantiki inaenda mbali zaidi kwa kuifafanua methali hii kuwa mtu yeyote anayejishughulisha hawezi kukosa riziki. Hivyo dai la kuwa pragmantiki huanzia pale ambapo semantiki huishia ndipo linapojidhihirisha.


“Aisifiaye mvua imemnyea” maana ya msingi au ya kisemantiki tunayoipata hapa ni kwamba anayeisifia mvua huwa imemnyeshea. Lakini pragimantiki inaendelea mbele zaidi kwa kuifafanua methali hiihii kuwa wepesi au uzito wa jambo anaujua yule liliyemkuta; ni vigumu sana kwa mtu ambaye hajafikwa na tatizo kuweza kuelewa uzito hasa wa tatizo hilo.


“Mkono mmoja hauchinji ng’ombe” katika methali hii maana ya kisemantiki ni kuwa mkono mmoja hauwezi kuchinja ng’ombe; lakini pragmantiki inaendelea mbali zaidi kwamba ili jambo lifanikiwe/ kufanikiwa kwa jambo kunahitaji ushirikiano.


“Mgema akisifiwa tembo hulitia maji” maana ya kisemantiki katika methali hii ni kuwa mtengenezaji wa pombe akisifiwa tembo (mnyama) hutia maji; hapa tunaona pragmantiki inaanzia hapo na kwenda mbali zaidi kufafanua methali hii kuwa mfanya jambo likaenda na sifa mweshowe hufanya tadi au jeuri.


Hivyo kutokana na methali hizo hapo juu msikilizaji kama atazingatia maana ya kisemantiki tu (maana msingi) hawezi kupata ujumbe uliolengwa na msemaji au mwandishi ipasavyo, hivyo ili kuupata ujumbe uliokusudiwa na mwandishi au msemaji atahitaji azingatie maana ya kipragmantiki na kwa kuzingatia maana ya kipragmantiki basi atauelewa ujumbe wa methali hizo vizuri hivyo kutokana na hilo tunathibitisha kuwa pragmantiki huanzia pale ambapo semantiki huishia.


            Matumizi ya semi mbalimbali; semi ni fungu la maneno linalotumiwa na jamii ya watu kwa namna maalumu ili kutoa maadili. Mfano wa semi;


“Biashara haigombwi” katika usemi huu maana ya msingi (kisemantiki) ni kuwa biashara haigombaniwi; lakini pragmantiki inaendeleza kutoka katika maana hii ya kisemantiki kwa kueleza maana ya methali hii kuwa ni busara mchuuzi kuwabembeleza wanunuzi wake.


“Cha mlevi huliwa na mgema” katika usemi huu maana ya kisemantiki ni kuwa kitu cha mlevi huliwa na mtengenezaji wa pombe, lakini pragmantiki inakwenda mbali zaidi ya semantiki kwani inafafanua maana ya usemi huu kuwa mali ya mtu asiyeithamini huwanufaisha watu wengine.


            Matumizi ya nahau mbalimbali, ni fungu la maneno lenye maana maalumu isiyotokana na maana ya kawaida za maneno hayo; katika nahau semantiki hutoa maana kulingana na maneno yaliyojitokeza katika nahau hiyo, hivyo huwa si rahisi kupata maana haswa iliyokusudiwa na msanii kwani ili kuipata maana hiyo ni shariti kurejelea maana ya kimuktadha (maana ya kipragmantiki) mfano wa nahau ni;


“Chinjia baharini” katika nahau hii maana ya msingi ni kuwa chinjia eneo lenye maji ya chumvi, hivyo kutokana na maana hii ya kisemantiki msikilizaji hawezi kupata maana ile iliyokusudiwa hivyo kutokana na hilo pengo pragmantiki inakamilisha kwa kuufafanua msemo huo kwamba ni nyang’anya au dhulumu.


“zunguka mbuyu ” maana ya ya kisemantiki katika nahau hii ni kitendo cha kugeuka kwenda upande mmoja wa mti mkubwa mnene sana wenye shina lenye nyuzinyuzi tu bila ya kubadili nafasi. Hivyo kutokana na maana hiyo ya msingi msikilizaji hawezi kupata maana hasa iliyokusudiwa na msemaji kwa maana hiyo tunaona kuwa pragmantiki inaenda mbali zaidi kuwa kuzunguka mbuyu ni kula rushwa.


 Pia ukweli wa dai hili kuwa pragmantiki huanzia pale semantiki inapoishia unaweza kudhihirishwa kwa kutumia mahusiano ya kifahiwa ambayo ni mahusiano ya maana ya maneno yanayounda kikoa kimoja cha maana kama ifuatavyo.


 Katika leksimu moja kuwa na maana nyingi zisizohusiana; mfano paa,kaa,pamba na panda ambapo kisemantiki maneno haya huwa na maana nyingi zisizohusiana na hivyo huleta utegemezi wa kimuktadha ili kupata maana kuntu na hapo ndipo pragmantiki inapofanya kazi iliyoachwa na semsntiki.


Vilevile katika semantiki kuna maneno ambayo huwa na maana nyingi zinazohusiana mfano “nguzo” na “mama” na hivyo uelewekaji wake hutegemea muktadha husika. Mfano neno “mama” maana yake ni asili, mzazi wa kike hivyo basi utumikaji wa neno hili katika sentensi huweza kuwa na maana tofautitofauti kulingana na muktadha. Mfano chuo cha Dar es salaam ni chuo mama hapa Tanzania.


Pia katika hali ya sentensi kuwa na maana zaidi ya moja au kueleweka kwa namna tofautitofauti ndipo pragmantiki hufanya kazi katika kueleza maana ya kimuktadha au maana ya ziada. Mfano,Juma anapanda hii inamaana ya kuwa;


Anasia mbegu


Anakwea mlima au mti


Sehemu ya tawi la mti


Hinyo basi katika kupata maana halisi ya manenoya namna hii hatuna budi kuhusisha na muktadha husika.


Ukweli mwingine wa dai hili tunaupata katika maneno ya ukinzani au vigambe viwili siganifu vinavyofanya kazi wakati mmoja; mfano, mtoto Yule ni mtu mzima kwelikweli.(+ mtoto,-mtoto) hapa maana ya kisemantiki ni kuwa mtoto huyu ni mtu mzima lakini pragmantiki inaenda mbali zaidi kwa kufafanua kuwa mtoto huyu anatabia za watu wazima mfano matendo yake; mfano mwingine ni kucheka huko ndiko kulia kwenyeweHivyo ubainishaji maana katika kauli hizi hutegemea muktadha ambapo neno hilo limetumika.


Vilevile dai hili huweza kuthibitishwa katika vimanilizi ambapo mtu hugundua maana ya jambo Fulani kupitia yanayosemwa na msemaji. Mfano( mazungumzo kati ya A na B)


a/ leo utaenda chuo


b/ sina kipindi


hivyo kutokana na mazungumzo hayo tunapata kimanilizi kuwa a/ hataenda chuo maana ambayo ni ya kipragmatiki na ambayo haielezwi na semantiki.


a/ vipi utaoga leo? 


b/ kuna baridi. 


Kutokana na mazungumzo hayo kimanilizi tunachokipata ni kuwa b/ hataoga maana isiyoelezwa na semantiki bali huelezwa na pragmantiki.


Kwa kuhitimisha ikumbukwe kwamba licha ya dai kuwa pragmantiki huanzia pale ambapo semantiki huishia hua na mashiko kwa kiasi Fulani lakini dhana zote mbili hutegemeana kwa kiasi kikubwa kwani maana ya ziada ambayo ndiyo ya kipragmatiki hujengwa au hutokana na maana ya msingi yaani maana inayochunguzwa na semantiki.


            MAREJEO


Bakari, N (1988),Analysis of Modern Swahili Texts and Language Skills. University of Nairobi.


Habwe, J na P. Karanja (2004), Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi. Phoenix publishes.


Stuwart, T na V. Nathan (2001), Language files ( 8th Ed).The Ohio State University.


Yule, G (1996), Pragmatic.London and New York.OUP


 


SWALI.


              Pragmantiki huanzia pale ambapo semantiki huishia. Hakiki ukweli wa dai hili kwa kutoa mifano murua na yakutosha kutoka katika lugha ya Kiswahili.     



Comments

Popular posts from this blog

KANUNI YA UAINISHAJI WA VITENZI (VERB SUBCATEGORIZATION)

Managing the Invisible Workforce: Freelancers, Bots, and Algoriths